Benin itaruhusu usafirishaji wa mafuta ya Niger kupitia bandari yake ya Seme, serikali ya Benin imesema Jumatano, ikitatua mvutano uliopo kati ya majirani hao wa Afrika Magharibi.
Niger ambayo haina bahari mwezi Novemba mwaka jana ilizindua bomba kubwa la kusafirisha mafuta ghafi kutoka kwenye kinu chake cha mafuta cha Agadem, kupitia Shirika la Taifa la Petroli la China (CNPC) kwenda nchi jirani ya Benin kwa usafirishaji kutoka Pwani ya Atlantiki.
Lakini upakiaji wa mafuta ya Niger katika bandari ya Seme Kpodji ulitatizwa na kufungwa kwa mipaka ya Niger na majirani zake wakati Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) ilipoweka vikwazo kufuatia mapinduzi ya Julai 2023 yaliyofanywa na jeshi la Niger.