Watu 18 wamefariki na wengine 33 kujeruhiwa baada ya basi walimokuwa wakisafiri kuanguka kwenye barabara inayopita juu ya mwamba, magharibi mwa Mexico.
Ofisi wa mwendesha mashtaka mjini Nayarit, ambapo ajali hiyo imefanyika, imesema kwamba basi hilo limeanguka kutoka urefu wa mita 15, jumamosi usiku.
Ajali ilitokea kwenye barabara kuu inayounganisha mji mkuu wa jimbo hilo wa Tepic na mji wenye shughuli za utalii wa Puerto Vallarta.
Maafisa wameripoti kwamba wanawake 11 na wanaume saba wamefariki.
Watoto 11 wanapatiwa matibabu hospitalini.
Wapiga picha wa wizara ya usalama na ulinzi wa raia wametoa picha zinazoonyesha waokoaji wakiwaokoa manusura kutoka kwa mabaki ya basi hilo.