Baraza la Mawaziri la Israel, Jumamosi limeidhinisha makubaliano ya kusitisha mapigano ya Gaza na kuachiliwa kwa mateka ambayo yatasimamisha vita vya miezi 15 na Hamas.
Serikali imetangaza mpango huo majira ya saa moja asubuhi kwa saa za Jerusalem baada ya baraza la mawaziri kukutana kwa zaidi ya saa sita na baada ya baraza la mawaziri la usalama Ijumaa kupendekeza mpango huo uidhinishwe.
Mkutano wa baraza la mawaziri ulifanyika kikamilifu kupita sabato ya Kiyahudi, ambayo huanza kwenye machweo ya Ijumaa.
Wakati wa Sabato, serikali kwa kawaida husimamisha shughuli zote isipokuwa katika hali za dharura za maisha na kifo, ikionyesha umuhimu wa makubaliano hayo.
Wakati huo huo, ving'ora vilivuma katikati mwa Israeli Jumamosi.
Maafisa wa jeshi la Israel walisema mifumo ya ulinzi ilitungua kombora lililorushwa kutoka Yemen.