Bahati nasibu ya Green Card DV - 2013

Bahati nasibu ya Green Card DV - 2013

Kipindi cha kujiandikisha kwa ajili ya bahati nasibu ya 2013 ilianza Jumanne Oktoba 4 na itamalizika Jumamosi Novemba 5 saa kumi jioni GMT

Kila mwaka Marekani hutoa visa 50 000 ya ukazi wa kudumu yaani Green Card kwa raia wa nchi zenye idadi ndogo kabisa ya wahamiaji hapa Marekani. Mpango huo hujulikana kama Diversity Visa Lottery DV, yaani bahati nasibu ya mchanganyiko wa raia.

Huo ni mpango ulioidhinishwa na bunge la Marekani na kusimamiwa na Wizara ya Mambo ya Nje.

Mtu yeyote anayeishi katika nchi hizo zenye wahamiaji wachache wanaotaka kuhamia Marekani kwa njia ya mpango huo anaweza kutembelea ukurasa wa tovuti ufuatao www.dvlottery.state.gov.

Kwa ujumla takriban watu wa mataifa yote ya dunia hushiriki katika bahati nasibu hiyo.

Kipindi cha kujiandikisha kwa ajili ya bahati nasibu ya 2013 kilianza Jumanne Oktoba 4 na kitamalizika Jumamosi Novemba 5 saa kumi jioni GMT

Kuna mabadiliko kadhaa kwa mpango wa mwaka huu kufuatana na naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayeshughulikia visa David Donahue.

Kwanza Sudan Kusini na Poland zitashiriki katika mpango wa 2013. Upande wa pili Bangladesh itaondolewa kutokana na kuwa na idadi kubwa ya wahamiaji Marekani.

Maombi yote yanabidi kufanyika kupitia tovuti kupitia ukurasa wa www.dvlottery.state.gov. Mtu akichaguliwa jina lake pia litatangazwa kwenye ukurasa huo na utaratibu wote utafanyika kwa tovuti. Ni muhimu kabisa kwa wanaoshiriki kuhifadhi nakala ya kila kitu wanachofanya na kuweka kila nambari za uthibitisho watakaopata baada ya kujiandikisha.

Ukurasa huo utakua mahala pekee ambapo mshiriki atapata habari kamili juu ya matokeo na ni mahali atakapofahamishwa ikiwa amechaguliwa wakati muafaka utakapofika.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani inawaonya watu kwamba ukipokea barua yeyote pepe inayodai unahitaji kulipa ada kuweza kujiandikisha basi huo ni utapeli kwa sababu hakuna ada inayotozwa kushiriki katika bahati nasibu hiyo. Watakaochaguliwa watalipa gharama za visa pekee yake katika ubalozi wa Marekani.

Wanaoshiriki wanabidi kufahamu kwamba wasisahau kuandika majina ya watu ambao ni familia yako yaani mkewe na watoto wako.