Baadhi ya raia wa Hong Kong na China watoroka nchini

Watu wakiaga jamaa na marafiki kwenye uwanja wa ndege wa Hong Kong kwenye picha maktaba

Baadhi ya wakazi wa Hong Kong na China bara ni miongoni mwa watu wanaotafuta njia ya kukimbia mateso huku wengine wakitafuta maisha mapya kwa ajili ya familia zao kwenye mataifa ya kigeni.

Inasemekana kwamba baadhi wamekimbilia Taiwan wakati wengine wakifanya safari ndefu kwenye mataifa kama vile Ecuador. Wahamiaji takriban 89,000 ambao ni sawa na asilimia 1 ya wakazi wa Hong Kong wanasemekana kuondoka kati ya 2020 na 2021, kwa mujibu wa data zilizotolewa na idara ya hesabu ya watu.

Mmoja wa wakazi wa Hong Kong Edwin Lai ameiambia VOA Jumatatu kwamba hali ya maisha mjini humo imeendelea kudorora na kwamba anatafuta mahala pengine pa kuhamia. Hali inasemekana kuharibika zaidi baada ya sheria mpya ya kitaifa ya kuwapeleka washukiwa wa Hong Kong kwenye mahakama za China bara sheria iliyopitishwa kati kati mwa mwaka jana baada ya miezi kadhaa ya maandamano.

Kuanzia wakati huo baadhi ya haki zinasemekana kuminywa kama vile kujieleza na elimu miongoni mwa nyingine. Mchora picha Kacey Wong ameiambia VOA kwamba ili kudumisha uhuru wake wa kujieleza,ni lazima aondoke Hong Kong.