AU yasikitishwa na uamuzi wa Russia wa kusitisha usafirishaji wa nafaka ya Ukraine

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat

Umoja wa Afrika Jumanne ulielezea maskitiko yake juu ya uamuzi wa Russia kusitisha makubaliano yanayoruhusu safari salama za meli za shehena za nafaka kutoka bandari za Ukraine za Black Sea.

.“Nasikitishwa na usitishwaji wa mpango wa nafaka ya Black Sea ambao Umoja wa Afrika umekuwa mtetezi wake wa mapema,” mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat alisema kwenye akaunti yake rasmi ya Twitter.

“Nazisihi pande husika kusuluhisha masuala yoyote ili kuanza tena usafirishaji salama wa nafaka na mbolea kutoka Ukraine na Russia hadi mahali bidhaa hizo zinapohitajika, hasa barani Afrika,” aliongeza.

Uvamizi wa Russia mwaka jana ulipelekea bandari za Ukraine za Black Sea kufungwa na meli za kivita hadi makubaliano yalipofikiwa chini ya upatanishi wa Umoja wa mataifa na Uturuki na kusainiwa mwezi Julai 2022, kuruhusu safari salama za meli za nafaka.

Jumatatu, Russia ilikataa kuongeza muda wa makubaliano hayo, ikitishia kupunguza usafirishaji wa chakula ambao tayari ulikuwa umepunguzwa, chakula ambacho watu walio katika hatari ya njaa, katika mataifa yanayoagiza nafaka yanakitegemea.

Makundi ya kibinadamu yanasema maeneo mengi ya Afrika yataathiriwa sana na hali hiyo, bara ambalo linategemea sana nafaka kutoka Russia na Ukraine, na ambako ma milioni ya watu tayari wanakabiliwa na viwango vya mzozo wa njaa.