Ilikuwa na Shangwe nderemo na vifijo baada ya timu ya Argentina kupata ushindi huo muhimu katika eneo la Funfest kulikojaa watazamaji wengi kushuhudia mchezo huo kati kati mwa jiji la Qatar.
Lionel Messi alikosa penalti iliyookolewa na kipa wa Poland Wojciech Tomasz Szczęsny anayecheza katika klabu ya ligi ya Serie A ya Juventus nchini Italia.
Argentina imefuzu baada ya kuwa vinara wa Kundi C wakitokea chini kabisa baada ya kupoteza mchezo wao wa kwanza na Saudia Arabia.
Poland pia ilifuzu kama washindi wa pili wa kundi hilo ingawa ushindi wa 2-1 wa Mexico dhidi ya Saudi Arabia katika mchezo mwingine wa kundi C ulimaanisha timu ya Poland inasonga mbele kwa tofauti ya mabao pekee.
Je Argentina watakirudia walichofanya mwaka 1990 ? ambapo walipoteza mchezo wao wa kwanza kwa kushtushwa na Cameroon lakini walienda mpaka fainali ya michuano hiyo.
Lakini pamoja na Lionell Messi kukosa penati katika mchezo huo washabiki wa Argentina waliimba jina la Mesi baada ya mchezo huo wakiwa wamejawa na furaha kubwa .
Magoli ya Argentina yalifungwa na na Alexis McAllister katika dakika ya 46 na Julian Albarez katika dakika ya 66.
Kwa maana hiyo Argentina sasa itakumbana na Australia katika raundi ya pili wakati Poland itakwaana na Ufaransa.
Poland pia pamoja na kufungwa imefanikiwa kuingia raundi ya pili baada ya Mexico kuwafunga Saudia Arabia bao 2-1 na Mexico kujikuta ina magoli mengi ya kufungwa licha ya kuwa pointi sawa na Mexico.
Nchi hiyo imefanikiwa kuingia raundi ya pili baada ya miaka 36.
Australia yavuka kuingia raundi ya pili
Nayo timu ya Australia -Socceroos imeshangaza ulimwengu wa soka baada ya kuitoa nje ya Mashindano hayo Denmark ilipoichapa bao 1-0 katika kundi D.
Australia haijawahi kuvuka raundi ya kwanza ya kombe la dunia katika miaka 16.
Timu hiyo ambayo haina wachezaji wowote wenye majina makubwa imeonyesha kucheza kwa moyo na umoja.
Australia sasa itakumbana na Argentina katika raundi ya pili.
Tunisia ya kwanza Afrika kutolewa kombe la dunia
Wawakilishi wengine wa Afrika timu ya Tunisia imekuwa ya kwanza kutolewa nje ya michuano hiyo mwaka huu licha ya ushindi dhidi ya mabingwa watetezi Ufaransa wa bao 1-0.
Ushindi wa Australia dhidi ya Denmark uliwapa Australia pointi 6 sawa na vinara Ufaransa na kuwaacha Tunisia na pointi 4 licha ya ushindi wao na kumaliza katika nafasi ya tatu.
Bao pekee la Tunisia lilifungwa na Wahbi Khazri katika dakika ya 58.
Tunisia walibaki wakiwategemea Denmark kutoka suluhu na Australia ili waweze kupata nafasi ya kusonga mbele katika kundi D.
Na alhamisi wawakilishi wengine wa Afrika Morocco wanafungua dimba na Canada wakati Croatia itapepetana na Belgium na mechi za mwisho zitakuwa ni kati ya Costa Rica na Ujerumani huku Japan itapambana na Spain.
Croatia Morocco na Belgium kila moja ana nafasi ya kusonga mbele katika kundi F isipokuwa Canada ambayo tayari imetolewa.
Mexico na Saudia Arabia nje ya kombe la dunia
Nayo timu ya Mexico licha ya kupata ushindi wa bao 2-1 dhidi ya Saudia Arabia imetolewa katika michuano ya kombe la dunia.
Timu hiyo inaungana na Saudia Arabia wote kwa pamoja wametolewa katika kundi C baada ya kumaliza katika nafasi ya tatu na ya nne mtawalia.
Mexico ilihitaji ushindi wa goli 3 na haikutakiwa kuruhusu goli lakini Saudia Arabia walipata goli moja na kupelekea Mexico kuwa na magoli mengi ya kufungwa kuliko Poland ingawa wako sawa kwa pointi na hivyo kutolewa nje ya mashindano hayo.