Dunia ya muziki inaomboleza kifo cha mwimbaji maarufu Aretha Franklin aliyekuwa akijulikana kama 'Malkia wa Soul' kutokana na sauti yake ya nguvu, yenye hisia zilizoanzia katika uimbaji wake wa nyimbo la gospel (za kidini).
Familia ya mwanamuziki huyo imetangaza kuwa amefariki saa tatu na dakika 50 asubuhi nyumbani kwake mjini Detroit Alhamisi akiwa amezingirwa na familia na marafiki. Alikuwa na umri wa miaka 76.
Taarifa ya familia inasema sababu ya kifo chake ni saratani ya kongosho. Kifo cha Aretha kimekuja siku chache baada ya vyombo vya habari kuanza kusema kuwa yupo katika hali mahtuti. Afya yake imekuwa ikidhoofika kwa miaka kadha iliyopita na mwaka jana alitangaza kuwa atawacha kufanya maonyesho.
Tangu kutangazwa kwa kifo chake mapema Alhamisi watu kadha nchini Marekani wamekuwa wakitokea katika televisheni za Marekani kuzungumzia jinsi Arethat alivyokuwa na ushawishi katika maisha na muziki nchini Marekani.
Mwanasiasa wa siku nyingi Jesse Jackson alisema katika mahojiano na CNN kuwa dunia imepoteza mtu muhimu sana katika dunia ya kisasa. Mwanamuziki Paul McCartney aliyekuwa katika kundi la Beetles aliandika katika ukurasa wake wa twitter, " Wote tuchukue muda mfupi kusema ahsante kwa ajili ya maisha ya Aretha Franklin......ambaye alituhamasisha kwa miaka mingi..."
Aretha Franklin ametawala ulimwengu wa muziki kwa karibu nusu karne nzima, huku nyimbo zake sio tu zikitamba katika chati bali kugeuka kuwa misemo katika maisha.
Nyimbo kama "Respect" uliandikwa na mwanamuziki mwingine Ottis Redding, "(You Make Me Feel Like) A Natural Woman," na wimbo "Think" ambao aliutunga na mume wake wa wakati huo Ted White ziligeuka kuwa nyimbo za kuwapa nguvu na hamasa wanawake duniani.
Aretha Franklin alikuwa mwanamke wa kwanza kuingia katika ukumbi wa Tuzo wa Rock and Roll Hall of Fame. Alishinda tuzo 18 za Grammy, ikiwa ni pamoja na mwimbaji bora wa R&B mwanamke kwa miaka minane mfululizo.
Familia ya Franklin inasema maelezo kuhusu maziko ya mwanamuziki huyo yatatangazwa karibuni.