Angola: Lourenco aelekea kushinda muhula wa pili, upinzani una mashaka na matokeo ya uchaguzi

Rais wa Angola Joao Lourenco, baada ya kupiga kura mjini Luanda, Agosti 24,2022. Picha ya AP

Rais wa Angola Joao Lourenco Alhamisi alitarajiwa kusalia madarakani, wakati chama chake kinaongoza katika uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali katika historia ya demokrasia ya nchi hiyo, huku karibu kura zote zikiwa zimehesabiwa.

Matokeo yaliyotangazwa na tume ya taifa ya uchaguzi yameonyesha chama tawala cha the People’s Movement for the Liberation of Angola (MPLA) kinaongoza kwa asilimia 51.7 ya kura huku asilimia 97 ya kura zikiwa zimekwisha hesabiwa.

Kura hizo ni ndogo sana ikilinganishwa na ushindi wake wa awali ambapo kilipata asilimia 61 ya kura.

Chama kikuu cha upinzani, the National Union for the Total Independence of Angola (UNITA) kinachoongozwa na Adalberto Costa Junior, kilipata asilimia 44.05, ikiwa ongezeko kubwa kutoka asilimia 26.67 kilizopata katika uchaguzi wa 2017.

Afisa mwandamizi wa chama cha UNITA ameuambia mkutano wa waandishi wa habari kwamba matokeo rasmi hayalingani na hesabu zao sawia.

“Tunatumai kunaweza kuwa na busara, hatuhamasishi uasi, mchakato haujamalizika, lazima tuwe watulivu,” amesema Anastacio Ruben Sicato.