Ikiwa ni 16% tu ya kura zilizohesabiwa na kutangazwa, hii ni inaonyesha baadhi tu ya matokeo kwa upigaji kura wa Jumatano. Matokeo ya mwisho ya kura ambayo yanaweza kuleta mabadiliko makubwa ya kisiasa katika demokrasia changa ya Afrika Kusini yalitarajiwa kuchukua siku kadhaa, huku tume huru ya uchaguzi ikisema yatatangazwa ifikapo Jumapili.
Waafrika Kusini wanasubiri kwa hamu kubwa kuona kama nchi yao, yenye uchumi wa juu zaidi barani Afrika, inaelekea kuona mabadiliko makubwa. Tume ya uchaguzi ilibashiri kuwa 70% ya wapiga kura wangejitokeza katika uchaguzi huu, kutoka 66% katika uchaguzi uliopita uliofanyika mwaka 2019. ANC kilipata ushindi wa 57.5% ya kura katika uchaguzi huo, licha ya utendaji wake mbaya zaidi, shirika la habari la AP limeripoti.
Uchaguzi huu ulionekana kama kura ya maoni ya moja kwa moja kwa utawala wa miaka thelathini wa ANC, ambao ulitoa uhuru kwa Afrika Kusini kutoka katika ukandamizaji, wa utawala wa kibaguzi katika uchaguzi wa kihistoria wa mwaka 1994 uliojumuisha watu wote , lakini umepungua umaarufu wake katika miaka 20 iliyopita. Mwaka huu unaweza kuwa ni wakati ambapo wananchi wengi wa Afrika Kusini wengi wanageuka kutoka ANC na kuinyima wingi wake kwa mara ya kwanza.
Matokeo yaliyotangazwa ni kutoka vituo vya kupigia kura 4,000 kati ya zaidi ya 23,000 katika majimbo tisa ya Afrika Kusini ambapo mchakato wa kuhesabu kura unaendelea. Takriban watu milioni 28 kati ya wakazi milioni 62 wa Afrika Kusini walisajiliwa kupiga kura.
Swali kubwa katika uchaguzi huu ni je, huu ni mwisho wa utawala wa ANC, baada ya utawala wa kibaguzi? Kura kadhaa za maoni zilionyesha kuwa ANC ilikuwa chini ya 50% kabla ya uchaguzi, hali isiyo ya kawaida.
Rais wa Afrika Kusini na kiongozi wa ANC Cyril Ramaphosa alisema baada ya kupiga kura Jumatano kwamba bado anaamini chama chake kitapata “wingi wa kutosha,” lakini kinakabiliwa na upinzani zaidi kuliko hapo awali.
Upinzani wa kisiasa umegawanyika kati ya vyama kadhaa, hata hivyo, ANC bado kinatarajiwa kuwa na viti vingi zaidi bungeni. Lakini ikiwa kura yake itashuka chini ya 50% kwa mara ya kwanza, kitahitaji muungano ili kubaki madarakani na makubaliano na wengine kumchagua tena Ramaphosa. Hilo halijawahi kutokea kabla.