Mahakama Kuu Marekani yaruhusu sehemu kubwa ya amri ya Trump

Rais Donald Trump

Mahakama kuu ya Marekani imesema kuwa itasikiliza kesi kuhusu amri ya kiutendaji iliyotiwa saini na rais Donald Trump.

Pia imefikia uamuzi juu ya amri inayokataza wasafiri- na ikaamuru kwamba sehemu kubwa ya amri hiyo, iendelee kutekelezwa kabla ya kesi hiyo kusikilizwa.

Amri hiyo ya Trump ambayo ilifanyiwa marekebisho, inawazuia watu kutoka nchi sita zilizo na Waislamu wengi, kuingia Marekani kwa muda wa siku 90.

Aidha amri hiyo ilisitisha program ya wakimbizi wanaonuia kuingia Marekani kwa kipindi cha siku 120.

Amri hiyo ilikuwa imesitishwa kwa muda na mahakama za rufaa, za majimbo ya Hawaii na Maryland. Maamuzi yote yaliendelezwa na mahakama za rufaa tofauti.

Hata hivyo, majaji wa mahakama kuu walisema kuwa amri hiyo haiwezi kutekelezwa kwa raia wa kigeni ambao wana uhusiano wa kweli na watu au taasisi za Marekani.

Mahakama ya juu ya kitaifa ilichukua msimamo tofauti, kwa kuruhusu katazo hilo litumike dhidi ya wasafiri wa Libya, Iran, Somalia, Sudan, Syria na Yemen na kusitisha programu ya wakimbizi.

Majaji hao hata hivyo wamesema katazo la kusafiri halitowaathiri “wananchi wa kigeni ambao wanamadai ya kweli ya kuwa na mahusiano na mtu au taasisi za Marekani.”

Mahakama ikaendelea kuelezea mahusiano yatayoidhinisha mtu kuruhusiwa kuingia Marekani: watu binafsi, wale walio na uhusiano wa kifamilia, wanafunzi, wanaoingia vyuo vikuu na vyuoni; wafanyakazi, waliopewa fursa ya kazi.

Trump amesema kuwa amri ya katazo la kusafiri litaanza kufanya kazi masaa 72 baada ya mahakama kutoa uamuzi.

Rais ameongeza kuwa uamuzi huo wa mahakama utailinda nchi. “Kama Rais, siwezi kuruhusu watu kuingia nchini ambao wanataka kutudhuru. Ninataka wale wanaoipenda Marekani na raia zake wote na wale ambao ni chapa kazi na wanazalisha katika taifa.”