Mbowe aliyekamatwa Julai 21 wakati akiwa kwenye hoteli moja mjini Mwanza, anakabiliwa na mashtaka ya kuhujumu uchumi na kutoa fedha kwa ajili ya kufadhili shughuli za ugaidi kati ya mwezi Mei na Agosti 2020. Mbowe alikamatwa wakati akijiandaa kuzindua kongamano la kushinikiza katiba mpya Tanzania.
Muda mfupi baadaye wafuasi kadhaa kutoka chama chake cha Demokrasia na maendeleo (Chadema) pia walikamatwa lakini kufikia sasa wameachiliwa bila kufunguliwa mashtaka yoyote.
Ripoti zinaongeza kusema kuwa kuna maandamano yaliyopangwa kufanyika leo kupinga kuendelea kushikiliwa kwa kiongozi huyo wa upinzani huku baadhi ya wakosoaji wakisema kuwa ni mwendelezo wa ukandamizaji dhidi ya wapinzani wa kisiasa.
Deprose Muchena, Mkurugenzi wa Shirika la Amnesty International, Mashariki na Kusini mwa Afrika amesema kuwa ni wakati wa kumuachilia kiongozi huyo mara moja.
-Imetayarishwa na Harrison Kamau, VOA, Washington DC