Aliyekuwa rais wa Burundi Pierre Buyoya amezikwa hii leo katika mji mkuu wa Bamako nchini Mali.
Buyoya ambaye alikuwa mwakilishi maalum wa umoja wa Afrika nchini Mali na katika kanda ya Sahel, alifariki dunia Desemba 18, alipokuwa anapata matibabu nchini Ufaransa. Alikuwa na umri wa miaka 71.
Familia yake ilisema kwamba Buyoya alifariki kutokana na maambukizi yta virusi vya Corona.
Viongozi wa Burundi hawakuhudhuria mazishi ya Buyoya katika makaburi ya kanisa katoliki mjini Bamako.
Baadhi ya viongozi wa zamani nchini Burundi wakati wa utawala wa Buyoya wamekosoa hatua ya serikali ya Burundi kutomuandalia mazishi ya heshima rais huyo wa zamani na badala yake kuzikwa nchini Mali.
Serikali ya Burundi ilimhukumu maisha jela Pierre Buyoya bila ya kuwepo mahakamani. Alishutumiwa kwa mauaji ya aliyekuwa rais Melchoir Ndadaye, shutuma ambazo alikanusha.
Buyoya aliongoza Burundi kati ya mwaka 1987 na1993, alipokabidhi madaraka kwa rais wa kwanza kutoka Kabila la Wahutu Melchior Ndadaye.
Ndadaye aliuawa katika mapinduzi ya kijeshi baada ya kuongoza kwa miezi mitatu.
Buyoya alirudi tena madarakani mwaka 1996 kupitia mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Rais Sylvestre Ntibantunganya, na kuongoza hadi mwaka wa 2003.
Alikuwa kiongozi wa mpito wa serikali ya muungano wa kitaifa, baada ya makubaliano ya amani yaliyosainiwa mjini Arusha, Tanzania mwaka wa 2000 yaliyomaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vya muongo mmoja vilivyosababisha vifo vya takriban watu 300,000.
Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC