Al Shabab yadaiwa kufanya mauaji Kenya

Kundi la kigaidi la Al-Shabaab limeua raia watano, wengine kwa kukatwaa vichwa, mashariki mwa Kenya, shahidi na chanzo cha polisi kiliiambia AFP, Jumapili.

Shambulio hilo lilitokea Jumamosi majira ya saa moja na nusu usiku katika vijiji vya Juhudi na Salama vya kaunti ya Lamu, ambayo inapakana na Somalia, afisa wapolisi amesema.

“Watu watano waliuwawa, huku wengine kwa kukatwa vichwa.”

Hassan Abdul, mkazi wa maeneo hayo amesema wanawake walifungiwa ndani ya nyumba na wanaume kuamriwa kutoka, ambapo walifungwa kamba na kuchinjwa.

Mwanafunzi wa shule ya sekondari ni miongoni mwa watu watano waliouawa, Abdul alisema, akiongeza kuwa wote waliouawa walikatwakatwa na baadhi yao walikatwa vichwa.

Mkazi mwingine wa vijiji hivyo, Ismail Hussein, alisema kuwa wanamgambo hao waliiba chakula kabla ya kuondoka, huku wakifyatua risasi hewani.

Wakitokea katika jirani ya Somalia, kundi la wanajihadi la Al-Shabaab limekuwa likiendesha uasi wa umwagaji damu dhidi ya serikali dhaifu ya Mogadishu kwa zaidi ya miaka 15.