Al Shabaab washambulia mji wa baidoa uliopo Somalia

Wafuasi wa kundi la wanamgambo wa al-Shabaab lenye makao yake nchini Somalia.

Mashahidi na maafisa wa usalama nchini Somalia walisema Jumamosi kwamba watoto wawili waliuwawa kufuatia shambulizi la bomu lililofanywa na wanamgambo wa al-Shabaab huko kusini-magharibi mwa Somalia katika mji wa Baidoa.

Mfanyakazi mmoja wa gari la wagonjwa, Yahya Isak Hassan alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kufika katika eneo la Hawlwadag mahala ambapo makombora yalipigwa. Aliiambia Sauti ya Amerika-VOA kwamba mizunguko 11 ya makombora ilipiga maeneo kadhaa na kuuwa watoto wawili, wote wasichana wenye umri wa miaka minne na mitano.

Hassan alisema msichana mmoja alifariki papo hapo kombora lilipopiga nyumba yao na mtoto wa pili alifariki akiwa hospitali. Watu 19 wengine walijeruhiwa katika shambulizi hilo.