Watoto 2 wa Akasha, raia 2 wa kigeni wasafirishwa Marekani kujibu kesi

Kutoka kushoto: Baktash Akasha, Gulam Hussein, Ibrahim Akasha na Vijaygiri Goswami

Serikali ya Kenya imewasafirisha kwenda Marekani washukiwa wanne wanaohusishwa na mtandao wa kimataifa wa madawa ya kulevya.

Baktash Akasha, Ibrahim Akasha, pamoja na raia wa Pakistan, Ghulam Hussein na Vijaygiri Goswami wa India walikamatwa Jumamosi.

Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili VOA ameripoti kuwa watu hao wanne wanatakiwa kujibu mashtaka katika mahakama moja ya New York, kwa kuhusishwa na ulanguzi wa biashara haramu ya madawa.

Vyanzo vya habari nchini Kenya vimesema kuwa afisa wa polisi na afisa wa upelelezi wamethibitisha kwamba watu hao wanne wamekwisha safirishwa kwenda Marekani kujibu mashtaka.

Maafisa hao hata hivyo wamekataa kutoa maelezo zaidi na kutaka majina yao yasitajwe kwani kesi za hao watu bado zinaendelea.

Watu hao wanne walitakiwa kuwepo mahakamani Jumatatu lakini wakili wao, Cliff Ombeta, akathibitisha kukamtwa kwao.

Wakili Ombeta alipeleka malalamiko Mahakama Kuu akitaka wateja wake wafikishwe katika mahakama hiyo, akieleza kuwa wameshikiliwa na hawana mawasiliano na mtu yeyote na kushikiliwa kwao ni kinyume na haki zao za msingi.

Wakili huyo pia amedai kuwa polisi watatu wa ngazi ya juu walihusika katika zoezi hilo la kuwakamata wateja wake.

Kufuatia maombi ya wakili, Jaji wa Mahakama Kuu, Njoki Mwangi amemtaka mkuu wa jeshi ya polisi, Joseph Boinnet na mkurugenzi wa makosa ya jinai, Ndegwa Muhoro kuwaleta watu hao wanne mahakamani.

Jaji Mwangi pia ametoa amri kusimamisha na kukataza maafisa wa polisi kuwaondoa watu hao wanne nchini, ambao walikuwa tayari wanakabiliwa na amri ya kusafirishwa nje ya nchi.

Imetayarishwa na Mwandishi wa idhaa ya VOA Josephat Kioko, Kenya