Airbus yasitisha utengenezaji wa ndege ya Superjumbo A380

Airbus A380

Kampuni hiyo kubwa na yenye makao yake nchini Uholanzi ilichukua hatua hiyo baada ya kutengeneza ndege ya Superjumbo kwa kipindi cha miaka 12.

Usitishwaji huo unafuatia hatua ya shirika la Ndege la Emirates, ambaye ndiye mteja mkubwa Zaidi wa Airbus380 kupunguza idadi ya ndege ilizoagiza kwa kiasi kikubwa.

Haya yanajiri wakati ambapo kulikuwa na matumaini makubwa ya kuimarisha usafiri wa ndege, huku kwa mamilioni ya abiria wakiendelea kutumia njia hiyo ya usafiri kila mwaka, huku mashirika mbalimbali ya Ndege yakieleza ugumu wa kujaza ndege ambazo zinabeba abiria kati ya 500 na 850.

Thomas Enders, Afisa mkuu, Kampuni ya Airbus alliambia shirika la habari la Reuters: "Ukiwa na bidhaa ambayo hakuna mtu anaitaka tena au unaiuza kwa hasara, basi hauna budi kusitisha utengenezajui wake, hata kama ni jambo la kusikitisha.

Hii ndiyo hatua inayofaa kuchukuliwa kwa sasa. Unaweza kuona kwamba hatukuvunjika moyao kwa haraka kuhusu A380. Tumefanya tathmini ya kina katika miaka ya karibuni. Ilifika mahali ambapo hatungepata wateja wapya au wateja wa kutosha kuinunua Ndege hiyo."

Wachambuzi wa masuala ya usafiri wa angani walikuwa wameonya kwamba kampuni hiyo haingerejesha mtaji iliyowekeza kwa mradi huo uliogharimu mabilioni ya dola kama haingeuza kati ya ndege 400 na 600.

Ndege moja ya Superjumbo, iliuzwa kwa dola milioni 446.