Wacongo na waafrika kwa ujumla waomboleza kifo cha msomi, mwanasiasa na mwanaharakati profesa Ernest Wamba dia Wamba, aliyefariki Mbanza Nugu huko Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo.
Wamba dia Wamba anakumbukwa kama mwanaharakati wa mwanzo kutetea mageuzi ya kidemokrasia, kuundwa kwa asasi za kijamii na siasa za kuwahusisha watu wote barani Afrika.
Alikuwa mhadhiri katika vyuo vikuu vya Dar es Salaam, Havard, Boston College na Brandeis hapa Marekani. Alishiriki katika vuguvugu la haki za kiraia hapa Marekani ambako alisomea masomo yake ya juu.
Aliporudi nyumbani alifungwa jela huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakati ilipokuwa inafahamika kama Zaire kabla ya kukimbilia uhamishoni Tanzania.
Aliporudi nyumbani Wamba Dia Wamba alichaguliwa Seneta katika bunge la Congo na kupewa wadhifa wa makamu rais wa kamati ya sheria na utawala ya baraza la Senate wakati wa serikali ya mpito.