Afrika Kusini: Zuma akosa kufika mahakamani

Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma.

Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma ambaye hivi karibuni alipewa msamaha na mahakama kwa misingi ya kimatibabu,Jumanne hakufika mahakamani wakati wa kuanza kusikilizwa tena kwa kesi inayomkabili, kuhusu ununuzi wa silaha mnamo mwaka 1999, wakati alikuwa makamu rais.

Viongozi wa mashtaka walielezea kutoridhika kwao na Zuma kutokuwepo katika mahakama kuu ya mjini Pietermaritz-burg kusini mashariki mwa jimbo la KwaZulu-Natal.

"Kuhudhuria mahakani siyo jambo la hiari," wakili wa serikali Wim Trengove, alisikika akisema.

Kesi hiyo, ambayo imekuwa ikiendelea kwa miaka mingi inahusu makubaliano ya ununuzi wa silaha za thamani ya dola bilioni 2, ambapo hii leo, timu ya wanasheria ilitarajiwa kutoa ombi la kumwondoa mwendesha mashtaka.

Kesi hiyo ilitarajiwa kuanza mwezi Mei mwaka huu, baada ya kukwama mara kwa mara na hoja za kisheria, lakini ilicheleweshwa tena na ombi la Zuma, kutaka mwendesha mashtaka mkuu Billy Downer aondolewe, kwa madai ya upendeleo.

Tarehe 7 mwezi Julai mwaka huu, Zuma, mwanye umri wa miaka 79, alifungwa jela kwa shutuma za kuidharau mahakama, na kupelekea ghasia mbaya zaidi na uporaji mbaya, ambao haukuwa umeshuhudiwa tangu kumalizika kwa utawala wa wazungu wachache, mnamo 1994, katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika. Zaidi ya watu 300 waliuawa, maelfu ya biashara kuporwa na mali nyingi kuharibiwa.