Afrika kusini imeingia wasiwasi kufuatia mashtaka ya Marekani ambapo ilisema maafisa walihonga taasisi ya mpira wa miguu duniani-FIFA ili kuwa wenyeji wa fainali za kombe la dunia mwaka 2010. Wizara ya michezo nchini Afrika kusini ilikanusha kwamba ilitoa malipo yeyote ili kuwa mwenyeji wa mashindano hayo ya kihistoria.
Mashtaka hayo yaliyotolewa na mwanasheria mkuu wa Marekani, Loretta Lynch yalipelekea kukamatwa hapo Jumatano kwa maafisa 14 wa FIFA na wakurugenzi ambao wanashutumiwa kukusanya na kupokea hongo ya zaidi ya dola milioni 150.
Mashtaka yaliyoelezewa na Lynch katika kurasa 164 yalielezea matukio ambapo makamu rais wa zamani wa FIFA, Jack Warner alimpeleka mtu Paris kukusanya sanduku lililojaa dola za Marekani kutoka kwa ofisa mmoja wa Afrika kusini. Mashtaka hayo hayakumtaja raia yeyote wa Afrika kusini kwa jina.
Sauti ya Amerika-VOA ilipojaribu kuwasiliana na maafisa wa Afrika kusini kutaka kujua matamshi yao msemaji wa rais wa Afrika kusini, Harold Maloka alirusha mpira huo kwa wizara ya michezo.
Waziri wa michezo Fikile Mbalula alisema kulingana na rekodi za maafisa hakuna malipo ya aina hiyo yaliyokuja kutoka kwenye wizara au serikali. “Rekodi zetu za fedha na vitabu vya fedha kwa mwaka 2010 na 2011, na vile vya kabla na baada ya kipindi cha Kombe la Dunia vimekaguliwa na mkaguzi mkuu wa mahesabu nchini Afrika kusini na hakuna kiasi hicho cha fedha ambacho kimegundulika kwenye vitabu vyetu”.
Chama kikuu cha upinzani nchini Afrika kusini tayari kimegeuza kashfa hiyo kuwa mpira wa siasa. Waziri kivuli wa michezo katika chama cha Democratic Alliance, Solly Malatsi, haraka alimkosoa mtu ambaye anafikiriwa sana kuwa kiini cha mkataba huu wa pembeni, Danny Jordaaan, mkuu wa kamati iliyopanga michezo ya ndani kwenye kombe la dunia mwaka 2010.
Jordaan hivi karibuni aliteuliwa kuwa mkuu wa meya wa eneo la Nelson Mandela Bay Metropolitan na chama tawala cha African National Congress-ANC. Alitarajiwa kuidhinishwa Alhamis. Simu zilizopigwa kwa ofisi ya meya hazikujibiwa.
Wakati Kombe la Dunia linafanyika nchini Afrika kusini, bwana Mandela alikuwa mgonjwa akiugulia nyumbani na aliweza kuhudhuria mara moja kwa muda mfupi kwenye hatua za mwisho za michezo hiyo. Msemaji wa taasisi ya Nelson Mandela alikataa kutoa matamshi yeyote juu ya mashtaka haya.