Benki ya Maendeleo ya Afrika -AFDB inalenga kuchangisha dola bilioni moja ili kuzuia mzozo wa chakula katika bara hilo uliosababishwa na uvamizi wa Russia nchini Ukraine, rais wake amesema.
Akiongea na Reuters siku ya Ijumaa Akinwumi Adesina alisema AFDB inapanga kuzindua mpango wa dharura wa uzalishaji wa chakula ambao utazingatia kukuza kwa haraka pato la ngano, mahindi, mchele na soya.
Mpango ni kuwa na uwezo wa kuzalisha takriban tani milioni 30 za chakula na kupeleka teknolojia mikononi mwa wakulima milioni 20, kwa hiyo unaangalia kiwango kikubwa na wakulima wadogo wadogo.
Kama sehemu kubwa ya dunia, nchi za Kiafrika zinakabiliwa na kupanda kwa bei ya bidhaa kwa kasi huku vita nchini Ukraine vikihatarisha usambazaji wa ngano na mahindi duniani na kupelekea bei ya mafuta kupanda.
Adesina alisema hiyo inafuatia janga la corona, ambalo tayari lilikuwa limesukuma watu milioni 24 zaidi katika bara hilo katika umaskini uliokithiri.