Raia kati ya 10 na 15 wameuwawa katika mashambulizi ya wikendi eneo la Beni mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ikiwa ni mashambulizi mapya yanayoaminiwa kutekelezwa na kundi la ADF linaloshirikiana na Islamic State, vyanzo vya ndani vimeeleza Jumapili.
“Kwa haraka serekali inatakiwa kukomesha ukatili huu,” Pepin Kavota, kiongozi wa mashirika ya kiraia Beni, mji ulioko kaskazini mwa jimbo la Kivu Kaskazini uliokumbwa na ghasia za ADF, aliiambia AFP.
Kavota aliongeza kuwa wengi wa walio uwawa walikatwa vichwa. “Kwa mwezi mmoja eneo letu limeathiwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya ADF,” alisema Antoine Kambale, afisa katika mji wa Mulekera, kaskazini magharibi mwa Beni.
Amesema raia 14 waliuawa Ijumaa katika maeneo kadhaa katika kitongoji hicho na shambulizi jipya limefanyika usiku wa Jumamosi mpaka Jumapili, huku wengine wawili wakiuwawa ambao ni mwanamke na afisa wa polisi.