ACT- Wazalendo chaomba Serikali kutoa maelezo kuhusu Rais

Rais wa Tanzania John Magufuli katika picha ya awali

Chama kikuu cha upinzani Tanzania cha ACT-Wazalendo Jumanne kimeitaka serikali kuelezea ni nani anaendesha nchi katika kipindi hiki ambacho Rais John Magufuli hajaonekana hadharani kwa zaidi ya wiki mbili sasa bila kuwa na maelezo yaliyotolewa kumhusu .

Kiongozi wa chama hicho ,Zitto Kabwe katika taarifa kwa vyombo vya habari amesema haijulikani mahali na hali ya Rais na wala umma haujaulishwa ni nani ambaye anasimamia uendeshaji wa ofisi ya yake katika kipindi hiki, na hivyo kuongeza hali ya sintofahamu.

Rais alionekana hadharani mara mwisho Februari 27 wakati akimuapisha Dr. Bashiru Ally kushika wadhifa wa katibu mkuu kiongozi, na baada ya hapo kumejitokeza ripoti mbali mbali za uvumi kuhusu hali ya afya ya yake.

Ijumaa iliyopita Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akitembelea wilaya ya Njombe alisema Rais anaendelea na kazi kama kawaida na kwamba ameongea naye kwa njia ya simu. Jumatatu Makamu Rais Samia Suluhu akiwa mkoani Tanga alisema kuwa huu ni muda wa kushikamana na kwamba ni kawaida kwa mtu kufanyiwa ukaguzi wa kiafya, na wala siyo jambo la ajabu kwa binadamu.

Majaliwa amewaomba wananchi kuchapa kazi kwa kuwa nchi taifa liko salama. Katika taarifa yake Zitto Kabwe amesisitiza kuwa wameridhisha kuwa Rais Magufuli ni mgonjwa na hivyo kuhoji kwanini serikali haisemi chochote kuondoa uvumi na kuelezea mi nani anayeongoza nchi kwa wakati huu.

Mtayarishaji : Harrison Kamau