Acacia yatuhumiwa kwa udanganyifu Tanzania

Rais John Magufuli

Serikali imeagiza kuwa kuanzia hivi sasa hakuna mchanga wa madini utakaoruhusiwa kutoka kwenda nje ya nchi.

Pia imeagiza kuwa kampuni ya uchimbaji madini nchini Acacia kutubu na kukubali makosa yake kama inataka kuendelea kufanya biashara nchini.

Rais John Magufuli ameagiza hayo na kuzitaka mamlaka zinazohusika kuiita kampuni hiyo na kabla ya jambo lolote, inapaswa kuilipa serikali fedha kwa kuwa imefanya udanganyifu kwa muda mrefu, na wakishakubali hayo tunaweza kukaa kwa makubaliano.

Ametoa kauli hiyo baada ya kupokea ripoti ya kamati ya pili iliyoundwa kuchunguza mchanga wa madini uliokuwa ukisafirishwa kwenda nje ya nchi, huku akiwataka wanasheria kuungana pamoja kwa ajili ya maslahi mapana ya Tanzania.

“Kwa kampuni hii inayojiita Acacia, muwaite kwanza muwadai hela zetu, kabla hata ya kusajili, wakubali kwamba tuliwaibia na tunatubu na tunalipa, tuko tayari kukaa kwa makubaliano, ninasema kwa sasa hakuna mchanga utakaotoka kwenda nje,” amesema rais Magifuli.

Aidha, Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi kuunda timu ya wanasheria waaminifu ambao watapitia na kuzifanyia marekebisho sheria zote zinazohusu mikataba ya madini ili zipelekwe bungeni kwaajili ya kujadiliwa na kufanyiwa marekebisho.

Amesema kuwa sheria hizo zinapaswa zipelekwe bungeni hata kama ni kwa bunge kuongezewa muda ili ziweze kujadili nakufanyiwa marekebisho kwa maslahi mapana ya Taifa. Aidha ameelezwa kushangazwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kushindwa kuwa na rekodi ya usafirishwaji wa dhahabu pamoja na Wizara ya Nishati na Madini kufanya kazi na kampuni ya Acacia bila kujua kama haijasajiliwa.

“Ukiwa na mali yako kwa mfano umepeleka pamba Ulaya, unapata rekodi kwamba safari hii tumepeleka tani kadhaa, je dhahabu, tunaona ni ya hovyo tu…Wizara ya Nishati haikujua kama inafanya kazi na mtu ambaye hajasajiliwa, unafanya nae kazi toka mwaka 1997, unawatuma TMAA wakamkague, hata siku moja hujawahi kumwambia wewe cheti chako kiko wapi,” amesema.