Abiy Ahmed ashutumu upinzani kujaribu kuigeuza Ethiopia kuwa kama Libya au Syria

Abiy Ahmed, Waziri Mkuu wa Ethiopia

Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed anatoa wito kwa wananchi kuunga mkono juhudi za vita akisema ushindi dhidi ya tishio la maadui zetu hauwezi kufikiwa ikiwa hatutafanya kazi pamoja

Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed katika taarifa yake ya maandishi anashutumu muungano wa upinzani kwa kujaribu kuigeuza Ethiopia kuwa Libya na Syria na kuongeza kwamba wamepanga kuiharibu nchi na sio kuijenga. Pia anatoa wito kwa wananchi kuunga mkono juhudi za vita akisema ushindi dhidi ya tishio la maadui zetu hauwezi kufikiwa, ikiwa hatutafanya kazi pamoja.

Kundi la Oromo linaloshirikiana na wapiganaji wa Tigray liliambia shirika la habari la AFP leo Jumatano, walipokuwa wakielekea kusini kwamba mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, unaweza kuvamiwa na wapiganaji ndani ya miezi kadhaa, kama sio wiki. Kundi la Tigray People’s Liberation Front (TPLF) ambalo limekuwa likipigana na serikali ya Waziri Mkuu, Abbiy Ahmed kwa mwaka mmoja limedai mafanikio makubwa katika siku za karibuni, pamoja na mshirika wake Oromo Liberation Army (OLA).

Odaa Tarbii, msemaji wa OLA kundi ambalo pia linadai maendeleo hivi karibuni huko Amhara na katika jimbo la Oromia linalozunguka Addis Ababa alisema kundi lake lilikuwa na nia ya kuiangusha serikali ya Abbiy, likitaja kuondolewa kwake kama hitimisho lisilotarajiwa. Kulingana na kituo cha FANA kinachomilikiwa na serikali, wabunge walitarajiwa kuidhinisha hali ya hatari leo Jumatano.