Abiy aamrisha mashambulizi Mekele baada ya muda wa kujisalimisha kumalizika

Mji wa Mekele, eneo la Tigray, Ethiopia

Waziri mkuu Abiy Ahmed, ameandika ujumbe wa twiter kwamba mlango wa mwisho wa amani ambao ulikuwa wazi kwa vikosi vya TPLF kutumia sasa umefungwa kabisa baada ya vikosi hivyo kudharau watu wa Ethiopia.

Mapema wiki hii, Abiy, ambaye alishinda tuzo la amani la Nobel mwaka uliopita kwa juhudi zake za kumaliza vita na migogoro ya kila mara kati ya Ethiopia na Eritrea, alitoa amri ya saa 72 kwa vikosi vya Tigray katika mji wa Mekele kujisalimisha la sivyo washambuliwe kijeshi.

Wanajeshi wa Ethiopia wamekuwa wakipigana na vikosi vya Tigray tangu Novemba 4, wakati Abiy alipotuma jeshi la ulinzi wa taifa katika eneo hilo baada ya vikosi hivyo kushutumiwa kwa kushambulia kambi ya jeshi la taifa.

Mamia ya watu wameuawa na zaidi ya 40,000 kukimbilia Sudan kama wakimbizi kutokana na vita hivyo wakisimulia hali mbaya katika eneo la Tigray.

Abiy amewaonya wakazi wa Mekele kuweka chini silaha na kusalia majumbani mwao.

Makundi ya kutetea haki yameelezea wasiwasi kuhusu vita hivyo, umoja wa mataifa ukitoa wito kwa waziri mkuu Abiy Ahmed kufanya mazungumzo na kumaliza vita hivyo kwa njia ya kidiplomasia.

Umoja wa mataifa umesema kwamba vita hivyo vimesababisha mateso mengi kwa watu wa eneo hilo ambao tayari wanakabiliwa na janga la virusi vya Corona.

Abiy amekataa pendekezo la kufanya mazungumzo.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC