Watu zaidi ya 100 wanasadikiwa wamepoteza maisha katika ajali ya meli iliyotokea kwenye kisiwa cha Chumbe kilometa chache kutoka Zanzibar. Meli ya MV Stargate ilikuwa katika safari yake ya kawaida kutoka Dar es Salaam kuelekea Zanzibar wakati wa ajali hiyo.
Baadhi ya abiria walionusurika katika ajali hiyo ambayo imetokea majira ya saa nane mchana wanasema awali meli ilipokuwa inayumba yumba kutokana na hali mbaya ya hewa baharini, mabaharia wa meli waliwaomba watu wawe watulivu, lakini hali ilizidi kuwa na mbaya na hatimaye meli hiyo ilipinduka.
Mmoja wa abiria Ali Faki Ali ambaye ni mfanyabiashara wa nguo anasema kabla ya meli kupinduka hali ndani ya meli miongoni mwa abiria ilikuwa ya mtafaruku mkubwa kwasababu kasi ya meli kuyumba ilikuwa kubwa sana. Bwana Ali anasema wao walifanikiwa kupanda juu ya mgongo wa meli na kwavile wanafahamu kiasi kuogolea waliweza kulifikia boya ambayo walilikamata kwa takriban saa mbili mpaka walipoweza kuokolewa na meli ya kikosi cha polisi Zanzibar.
Wakati huo huo, naibu waziri wa mawasiliano na uchukuzi wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar, Issa Haji Gave ambaye alikuwa katika eneo la ajali anasema kwa mujibu wa orodha rasmi ya meli hiyo kulikuwa na abiria takriban 281, ambapo abiria 250 walikuwa watu wazima na watoto 31. Mpaka sasa watu walionusurika katika ajali hiyo ni abiria 134 na maiti nane ndiyo zimeweza kupatikana na maiti hizo ni za watoto wadogo.
Meli hiyo inamilikiwa na mfanyabiashara Saidi Mbuzi ambaye mwaka 2009 alipoteza meli nyingine ya MV Fatih ambayo ilizama karibu na bandari ya Zanzibar.