Soko la Afrika Mashariki kuanza kazi mwakani?

Nchi za Afrika Mashariki na Kati zinatarajiwa kuwa na sarafu moja mwaka 2012, hatua ambayo Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Dr. Deodurus Kamala, anasema itakuwa miongoni mwa maswala makuu ya ushirikiano wa nchi hizo.

Dr. Kamala ambaye ndiye mwenyekiti wa baraza la mawaziri wa Jumuia hiyo kwa sasa, anasema soko la pamoja kwa nchi hizo litaanza mwezi Julai mwakani, baada ya mabunge ya nchi wanachama kuridhia mkataba wa protokali uliotiwa saini na marais wa Jumuia hiyo Novemba mwaka huu.

Katika soko hilo la pamoja kila nchi itafungua sehemu ya ajira kwa wananchi wa Afrika Mashariki, na kwa kuanzia nchi hizo zitaanza na sekta binafsi, kama vile madini, viwanda, na sekta nyingine zisizo rasmi katika nchi hizo.

Kwa upande wa Tanzania Dr. Kamala amesema Zanzibar haitahusishwa katika awamu ya kwanza ya soko huru la nchi hizo, lakini hakutaja sababu kwa nini visiwa hivyo ambavyo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania havihusiki na protokali hiyo ya awali.