Kenya yazindua mitambo ya Televisheni ya Digitali

Kenya imekuwa ni nchi ya pili barani Afrika baada ya Afrika Kusini kuzindua mfumo wa teknolojia ya utangazaji wa televisheni kwa kutumia mitambo ya digital kama ilivyo kwenye mataifa yaliyoendelea .

Hii ina maana kwamba kuanzia mwezi Juni mwakani vituo vyote vya utangazaji wa televisheni nchini Kenya vitatumia mfumo huo mpya wa utangazaji baada ya kuondolewa kwa mfumo wa sasa wa analog.

Rais wa Kenya Mwai Kibaki alizindua mfumo huo na kusema kuwa uzinduzi wa mfumo huo ni muhimu sana kwasababu utaiweka nchi ya Kenya katika upeo mpya wa utangazaji.

Afrika Kusini ilikuwa nchi ya kwanza kupata mitambo hiyo barani Afrika. Wataalam na waandishi wa utangazaji wamesema Kenya imelazimika kuzindua mfumo huo ili kutekeleza agizo la shirika la mawasiliano duniani (ITU) yanayotaka mataifa yote duniani kuzingatia mfumo huo wa utangazaji ifikapo 2015.