Wabunge Kenya wamtaka Mudavadi ajiuzulu

Wabunge nchini Kenya wamemtaka naibu waziri mkuu Musalia Mudavadi ajiuzulu kufuatia madai ya kuhusika katika kashfa ya ununuzi wa ardhi ya makaburi ambapo maafisa waliweza kutumia mradi huo kufuja mamilioni ya fedha za umma.

Joto la kisiasa dhidi ya Mudavadi, ambaye pia ni waziri wa serikali za mitaa na mabaraza ya wilaya linaendelea kupamba moto siku hadi siku, baada ya wabunge kuendelea kutoa shinikizo kali la kumtaka ajiuzulu kufuatia kashfa ya ununuzi wa ardhi kwenye viunga vya jiji la Nairobi. Lakini kiongozi huyo amejitetea vikali kutokana na shutuma hizo na ametangaza kuwa hatajiuzulu wadhifa wake.

Baadhi ya wabunge wamesema kuwa ripoti ya tume ya taifa ya kupambana na ufisadi nchini humo imeonyesha wazi wazi kashfa hiyo ambapo wananchi wa Kenya walipoteza mamilioni ya fedha na haiwezi kutekelezwa bila kiongozi huyo kujiuzulu.

Tofauti zilizopo katika serikali ya mseto nchini Kenya zimepelekea kufukuliwa kwa kashfa katika wizara mbali mbali ambapo mamilioni ya fedha za umma yametumiwa kiholela. Duru zinasema huu ni mwanzo tu wa mapambano makali ya kisiasa kati ya vyama vya ODM na PNU, kwani tayari viongozi wa vyama hivyo wameunda mizizi ya kuchimba kashfa na kusambaza habari hizo zinazoonyesha wapinzani wao kama mafisadi sugu.