Rais wa kenya, Mwai Kibaki amewapiga marufuku mawaziri katika baraza lake kusafiri nje ya nchi wakati bunge la Kenya linajitayarisha kujadili rasimu ya katiba mpya.
Katika taarifa iliyotolewa jana, msemaji wa serikali, Alfred Mutua amesema waraka wa rais uliosambazwa unawazuia mawaziri wote na mawaziri wadogo kusafiri nje ya nchi ili kuhakikisha kuwa wanahudhuria mijadala yote katika bunge.
Mjadala kuhusu katiba unatarajiwa kuanza haraka na utadumu kwa siku 30 katika bunge, kabla ya waraka huo kuwasilishwa kwa wananchi upigiwe kura.
Utaratibu wa tathmini ya katiba unaonekana na wakenya wengi kuwa ni hatua muhimu katika kuepuka ghasia za uchaguzi.
Kenya kwa wiki kadhaa ilikumbwa na ghasia na mapigano ya kikabila baada ya uchaguzi wa rais wa mwaka 2007 uliomalizika kwa Bwana Kibaki kutangazwa mshindi katika matokeo yaliyokuwa na utatanishi.
Zaidi ya watu 1300 waliuwawa na takriban watu laki 3 walipoteza makazi yao kabla ya ghasia kudhibitiwa.