Waziri wa Ulinzi Somalia anusurika na shambulizi la Al Shabab

Waziri wa ulinzi wa Somalia Yusuf Mohamed Siyad amenusurika na mashambulizi mawili ya mabomu katika mji mkuu Mogadishu.

Kundi al Alshabab limedai kuhusika na shambulizi hilo la Jumatatu dhidi ya waziri wa Ulinzi wa Somalia Yusuf Mohamed Siyad ambaye pia anajulikana zaidi kama “Inda' Ade”.

Mashahidi wanasema bomu la kwenye gari na kifaa cha mlipuko kandoni mwa barabara kililipuka kwenye barabara ya Maka Al-Mukarama. Barabara hiyo inaunganisha jumba la Rais na uwanja wa ndege wa Mogadishu na hutumiwa mara kwa mara na viongozi wa serikali ya Somalia.

Mogadishu imepata ongezeko jingine la mashambulizi wakati serikali ikijiandaa kufanya mashambulizi dhidi ya makundi ya waasi wa kiislam.