Wakili Marando:Babu Seya aweza kuokolewa tu na msamaha wa Rais

Baada ya mahakama ya rufaa nchini Tanzania kukataa rufaa ya mwanamuziki mashuhuri nchini humo, Nguza Viking - maarufu kama Babu Seya – ni wazi kuwa mwanamuziki huyo na mwanae mmoja Papii Kocha ambaye pia ni mwanamuziki wa kizazi kipya watamalizia maisha yao gerezani.

Watoto wengine wawili wa Babu Seya - Francis Mbangu na Nguza Mashine – waliachiliwa huru baada ya kuonekana na mahakama ya rufaa hawana makosa yoyote baada ya kukaa gerezani kwa miaka sita. Babu Seya na watoto wake hao watatu wa kiume walihukumiwa kifungo cha maisha baada ya kukutwa na hatia katika mashitaka mbali mbali ya ubakaji.

Sauti ya Amerika imezungumza na mwanasheria wa kujitegemea wa Babu Seya, Mabere Marando, ambaye amesema kufuatia hukumu ya mahakama ya rufaa njia pekee iliyobaki ambayo inaweza kuwatoa Babu Seya na Papii Kocha gerezani ni msamaha wa rais tu.