Balozi wa Kenya apewa cheo cha UN

Balozi wa Kenya katika Umoja wa Mataifa Zachary Muburi –Muita, ameteuliwa kuwa rais wa kamati ya ushirikiano wa nchi za kusini kwa muda wa miaka miwili. Kamati hiyo inajukumu la kusimamia utungaji wa sera za kiserikali na hukutana mara mbili kwa mwaka. Maamuzi ya kamati hiyo pia huidhinishwa na baraza kuu la Umoja wa Mataifa.

Akizungumza na sauti ya Amerika kutoka New York, Balozi Muita alisema atahimiza ushirikiano wa karibu zaidi kati ya nchi za Kusini na Kaskazini katika maswala ya kiuchumi na maendeleo. Alisema uteuzi wake pia ni heshima kubwa kwake binafsi, taifa la Kenya na Afrika kwa jumla. Alisema masoko ya nchi za Afrika hupoteza kiasi kikubwa cha fedha kutokana na hali duni ya kiteknolojia, swala ambalo atalipa kipaumbele na kuomba nchi zingine za Kusini kama vile Brazil, India na China kusaidia.

Wakati huo huo, Balozi Muita alisema amefurahia uamuzi wa Umoja wa Mataifa wa kuinua ngazi ya mji wa Nairobi kutoka kundi la ‘C’ hadi la ‘B’ akisema hili limetokana na kuimarika kwa hali ya maisha katika mji mkuu wa Kenya.

Alisema maamuzi hayo yatasaidia Kenya katika sekta ya utalii na kuvutia waandalizi wa kongamano za kimataifa kuchagua mji huo kwa shughuli zao.