Mrepublican ahoji usaili wa Abdulmutallab

Seneta mwandamizi wa chama cha Republican katika bunge la Marekani amehoji namna serikali ya Obama ilivyochukua hatua dhidi ya Mnigeria Umar Farouk Abdulmutallab, 23, baada ya kumkamata alipojaribu kulipua ndege ya Marekani Disemba 25. Katika hotuba ya kila wiki Jumamosi Seneta Susan Collins alielezea kushtushwa kwamba wapepelezi wa serikali walitumia dakika 50 tu kumhoji mtuhumiwa huyo kabla ya kumruhusu akutane na mwanasheria aliyepewa na mahakama.

Seneta Collins anasema shirika la FBI lilimchukulia Abdulmutallab kama mhalifu wa kawaida badala ya gaidi kutoka nje ya nchi kama anavyoshukiwa, bila kushauriana na idara za taifa za upelelezi. Seneta huyo alisema uamuzi huo ulikuwa wa hatari na ameushutumu utawala wa Obama kuwa na upofu kiasi katika kupambana na ugaidi wa kimataifa.

Abdulmutallab ni raia wa Nigeria anayeshutumiwa kwa kujaribu kulipua ndege ya shirika la Marekani wakati inakaribia kutua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Detroit kutoka Amsterdam Disemba 25.