Uvutaji Sigara Afrika Mashariki na Kati









Uvutaji sigara Afrika Mashariki na Kati ni tabia ambayo imekuwa ikipungua katika baadhi ya maeneo na kuongezeka katika sehemu nyinginezo. Kwa miaka kadha sasa wanaharakati wamekuwa wakipiga vita tabia hiyo kutokana na athari zake katika afya ya mtu na jamii kwa jumla.

Nchini Kenya serikali imechukua hatua kadha kupunguza tabia ya uvutaji ikiwa ni pamoja na kuweka masharti makali katika matangazo ya sigara na bidhaa nyingine za uvutaji na pia kuzuia uuzaji wa sigara moja moja kwa lengo la kufanya tabia hiyo iwe ya gharama kubwa mtu anapolazimika kununua paketi nzima. Hata hivyo, ingawa kuna dalili za upunguaji wa uvutaji wasiwasi upo hasa kwa vijana wanaoanza kuvuta sasa. Imedhihirika pia kuwa idadi kubwa ya wanawake wanavuta sigara tena hadharani kuliko ilivyokuwa katika ya nyuma.

Huko Tanzania wanaharakati waliandamana mbele ya ofisi za jiji la Dar es Salaam na Wizara ya Afya Novemba mwaka jana kuwasilisha madai ya kutaka serikali ichukue hatua kali zaidi katika masharti ya utangazaji wa bidhaa za tumbaku. Uganda pia imepiga hatua kubwa katika masharti ya matangazo ya bidhaa za tumbaku lakini uvutaji sigara ungali katika kiwango cha juu. Sikiliza makala hii maalum kuhusu uvutaji Afrika Mashariki na Kati.