Serikali ya Kenya imetishia kumuondoa Rais mstaafu Daniel Arap Moi na watu wengine mashuhuri kutoka mashamba makubwa waliochukua kwa njia isiyo halali katika msitu wa Mau, uliopo kwenye jimbo la Rift Valley nchini humo.
Siku za hivi karibuni serikali ya Kenya imekabiliwa na shutuma kali kutoka kwa viongozi wa serikali na raia wa kawaida waliopewa mashamba yasiyo halali katika msitu huo wa Mau.
Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga, amesema wakati umefika kuwaondoa watu hao mashuhuri waliohusika kuchukua maeneo kinyemela katika msitu huo. Tayari serikali imeanza kuwafukuza watu waliochukua mashamba hayo licha ya pingamizi kutoka kwa wabunge wa eneo hilo.
Bwana Odinga ambaye amekuwa mstari wa mbele katika juhudi za kuhifadhi msitu huo, anasema watu wote waliovamia msitu huo na kuharibu chemchem zote za maji ni lazima waondoke kwa hiyari yao wenyewe na hatimaye kusaidiwa na serikali kupata makazi mapya.
Waziri mkuu huyo amesema watu hao maarufu wamekuwa wakiwachochea watu kupinga juhudi za serikali za kuondolewa kwenye msitu huo, ili waweze kunufaika na mashamba hayo.