WHO: Idadi ya watoto wanaokufa kutokana na Malaria yapungua

Shirika la Afya Duniani – WHO - linasema watoto wachache wanakufa kutokana na malaria, kwa sababu ya matumizi ya vyandarua vilivyonyunyiziwa dawa na matibabu bora.

Wakati hatua muhimu zikifanywa, WHO inasema mpango wa malaria lazima uimarishwe kufikia malengo ya maendeleo ya millennium ya Umoja wa Mataifa, MDG's kupunguza nusu ya vifo vitokanavyo na malaria ifikapo mwaka 2015.

Ripoti mpya ya WHO kuhusu Malaria kwa mwaka 2009, inajumuisha takwimu kutoka nchi 108. Shirika hilo linaripoti nusu ya idadi ya watu duniani wapo kwenye hatari ya kupatwa na malaria. Kiasi cha kesi milioni 243 za malaria zilitokea mwaka jana, na kuuwa takribani watu laki tisa. Wengi wa watu waliokufa walikuwa watoto katika nchi zilizo chini ya jangwa la Sahara barani Afrika.

WHO inasema fedha inaweza kuleta tofauti kati ya maisha na kifo. Mwaka huu jumuiya ya kimataifa ilitoa dola bilioni moja nukta saba, ambapo ni zaidi ya mara mbili ya kiwango ambacho kilitolewa mwaka 2006.

Mkurugenzi wa mpango wa malaria wa WHO, Robert Newman, anasema msaada zaidi wa fedha umewezesha uwezekano wa kusambaza vyandarua zaidi vilivyonyunyiziwa dawa ili kuokoa maisha na kuwatibu watu wasiojiweza.

Anasema mafanikio makubwa yamepatikana katika maeneo ambayo hatua za udhibiti wa ugonjwa huo zimeongezeko.