Maiti za watu 19 zilizopatikana kufuatia maporomoko ya ardhi yaliyosababishwa na mvua kubwa zilizotokea katika kijiji cha Goha, huko Same katika mkoa wa Kilimanjaro nchini tanzania wamezikwa Alhamisi.
Miongoni mwa maiti hizo ni pamoja na wanaume, wanawake na watoto wadogo wenye umri kati ya miaka 2 mpaka 12. Taarifa zinasema maiti hizo ni kati ya watu 25 waliodaiwa kupotea zinatoka katika vijiji vya Kambeni na Goha katika wilaya ya Same.
Kulingana na mwandishi mwandamizi wa jeshi la Polisi nchini Tanzania Mohamed Mhina, tukio hilo lilisababishwa na mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia Jumatano na kupelekea nyumba zilizo kando kando ya mlima Manka kuangukiwa na miamba na udongo mzito ambao ulikusanya miti mikubwa na kuteketeza kabisa nyumba saba katika eneo hilo.
Mhina amesema kazi bado inaendelea kutafuta miili ya watu inayohofiwa kuwa huwenda bado ipo kwenye vifusi hivyo, lakini hakuna vifaa maalum vya kuweza kusaidia kutoa matope kwa urahisi na mawe makubwa yaliyodidimia kwenye ardhi. Amesema watu wanatumia vifaa vya kawaida kama mabereshi na majembe kutafuta miili ya watu.