Wauaji wa Albino wahukumiwa vifo

Mahakama kuu nchini Tanzania katika kituo cha Shinyanga, Jumatatu imetoa adhabu ya kunyongwa kwa watu wanne baada ya kupatikana na hatia ya kumuuwa mtu mwenye ulemavu wa ngozi-Albino, kwa kumkata kichwa na miguu yote miwili.

Akitoa hukumu hiyo jaji Gadi Mjemas, alisema mahakama imeridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka kuwa washtakiwa wote kwa pamoja walikula njama na kumuuwa kwa makusudi Lyaku Wile, ambaye alikuwa mlemavu wa ngozi-Albino.

Alisema ushahidi huru uliotolewa na mkemia mkuu wa serikali kuwa vinasaba vya marehemu vilikutwa katika panga na kisu, vifaa vilivyotumika kwenye mauaji hayo vilishabihiana na vinasaba vya watu hao. Washitakiwa hao Imboje Mawe, Chenyenye Kishiwa, Sai Gamaya na Sai Mafizi wote wakazi wa kijiji cha Kindabwiye, kilichopo Bariadi mkoani Shinyanya, walifikishwa mahakamani Mei 8 mwaka huu.

Hii ni hukumu ya pili kutolewa nchini Tanzania kwa watu waliopatikana na tuhuma za kuuwa watu wenye ulemavu wa ngozi-Albino. Katika miaka ya karibuni mauaji ya Albino yalipamba kasi katika mikoa ya kanda ya ziwa kutokana na imani potofu, kwamba viungo vya Albino vinaweza kumpatia mtu utajiri na hata kumuongezea bahati katika maisha yake.