Al-Shabab wajaribu kumshambulia rais wa Somalia

Wakazi ambao wamezoea mapigano katika mji mkuu wa Mogadishu wameleza mapigano ya asubuhi ya Alhamisi kati ya vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika, AMISOM na wanamgambo wa Al-Shabab, kua ni moja wapo ya mapigano ya kutisha walowahi kushuhudia.
Shahidi mmoja Mohamed Ali ameiambia Sauti ya Amerika alikua karibu na kufungua duka lake karibu na soko kuu la Bakara wakati mizinga ilipoanza kuporomoshwa kutoka kila upande.
“Wafanya biashara na wanunuzi mara moja wakaanza kukimbia kwa hofu wakati mizinga ilipoanza kusikika. Baadhi ya watu waliuliwa na wengine kujeruhiwa walipokua wanatafuta mahali pakujificha.”


Mapambano hayo ya leo yalianza wakati Rais wa serekali ya mpito, inayoungwa mkono na Jumuia ya Kimataifa Sharif Sheik Ahmed alipokua anajitayarisha kuelekea Uganda ili kuhudhuria mkutano wa Umoja wa Afrika juu ya wakimbizi na wakazi walokimbia makazi yao wanaoishi ndani ya nchi zao IDPs. Waandishi wa habari wa mji huo wanasema, wanamgambo wa Al-Shabab walifyetua mizinga kwenye uwanja wa ndege na kuwasababisha walinda amani wa kikosi cha AMISOM kujibu vikali.

Wafanyakazi wa huduma za afya wanaripoti kua wengi ya watu walofariki na kujeruhiwa walikua ndani ya soko la Bakara. Wanasema maeneo mengine mawili ya mji yanayoshikiliwa na Al-Shabab yalishambuliwa pia.

Kufuatana na waandishi wa habari wa kisomali majeshi ya AMISOM mara kwa mara hushambulia soko la Bakara na ngome nyingine za Al-Shabab katika mji mkuu. Wanamgambo wamekua kwa muda mrefu wakitumia maeneo haya kufanya mashambulio yao ya mizinga dhidi ya vituo vya AMISOM, ambavyo ni uwanja wa ndege, bandari na ikulu ya Rais.
Mfanyabiashara Ali anasema walinda amani mara kwa mara hujibu kiholela holela na kusababisha majeruhi miongoni mwa wakazi.

“Wanamgambo wa kislamu wanasababisha matatizo kwa kuwashambulia walinda amani, lakini AMISOM wanajibu vikali na hivyo kusababisha hasara kuliko ulinzi.”
Ali anaionya AMISOM kua wananchi huwenda wasistahmiliye tena kuwepo kwao huko Somalia ikiwa wataendelea kushambulia maeneo ya raia. AMISOM imekua daima ikikanusha tuhuma kama hizo. Akizungumza na Idhaa ya Kisomali ya Sauti ya Amerika msemaji wa AMISOM alisema kua Al Shabab hufanya mashambulio yake kutoka soko la Bakara ili kuongeza chuki za raia dhidi ya AMISOM.