Bunge la Kenya lamkataa Jaji Ringera

Bunge la Kenya limekataa kuidhinisha uteuzi wa Jaji Ringera, kama mwenyekiti wa tume ya kupambana na rushwa nchini humo. Uteuzi uliofanywa hivi karibuni na Rais Mwai Kibaki. Bunge la nchi hiyo linadai Rais Kibaki amevunja sheria katika uteuzi huo.

Rais Kibaki amefedheheshwa na uamuzi wa bunge kupinga hatua ya uteuzi huo pamoja na wasaidizi wake wawili. Katika majadiliano makali yaliyoendelea hadi saa tatu usiku, saa za Afrika Mashariki, upande wa serikali ulishindwa kulishawishi bunge kuhusu uteuzi huo wa Jaji Aaron Ringera.

Zaidi ya wabunge 84 waliupinga uteuzi huo dhidi ya wabunge 45 wa upande wa serikali. Upande wa serikali ukiongozwa na Waziri wa Miradi Maalum, Dr. Naomi Shaban, ulidai mzozo huo unastahili kuwasilishwa mahakamani, kwasababu bunge halina uwezo wa kikatiba kusuluhisha mzozo huo.

Dr.Naomi Shaban pia aliwasihi wabunge kumheshimu Rais Kibaki juu ya uteuzi huo. Lakini wabunge wengi walioshiriki kwenye majadiliano hayo walinukuu sheria za bunge la Marekani na Uingereza, ili kuwashawishi wenzao kuwaunga mkono na kuendelea kupinga uteuzi huo. Wengine walinukuu Biblia na Korani tukufu.