Rais Mwai Kibaki wa Kenya amefanya mabadiliko katika jeshi la polisi na kumwondoa Kamishna mkuu wa polisi, Meja Jenerali Hussein Ali, na nafasi yake kuchukuliwa na Mathew Iteere ambaye alikuwa kamanda wa kikosi cha GSU. Hatua hii ya Rais Kibakiinafuatia shinikizo kutoka ndani na nje ya nchi juu ya utendaji kazi wa jeshi la polisi nchini Kenya.
Tangazo hilo la ghafla kutoka ikulu ya Nairobi limetolewa wakati rais Kibaki anakabiliwa na lawama kali kutoka mashirika ya haki za binadamu, mshauri wa kisheria wa Umoja Mataifa, Profesa Phillip Alston, wanasiasa na wananchi kuhusu utendaji kazi wa Meja Hussein Ali. Chini ya uongozi wake jeshi la polisi Kenya limeshutumiwa na visa vya mauaji ya kikatili yanayofanywa na idara hiyo.
Waziri mkuu wa Kenya Raila Odinga amekuwa katika mstari wa mbele kati ya viongozi waliohimiza kufutwa kazi kwa kamishna mkuu wa polisi Hussein Ali, kama hatua mojawapo ya kuangamiza ufisadi serikalini. Bwana Odinga alisema anataka kuleta mabadiliko katika kikosi cha polisi, ili polisi waweze kuwahudumia wananchi kwa usawa. Bwana Ali sasa atakuwa mkuu mpya wa idara ya posta.