Uchaguzi Gabon waleta utata.

Wagombea watatu wa uchaguzi wa urais nchini Gabon wote wanadai ushindi, ingawa hakuna matokeo rasmi yaliyotangazwa tangu upigaji kura ufanyike siku ya Jumapili.

Ali Ben Bongo, mtoto wa kiume wa marehemu rais Omar Bongo, alisema leo Jumatatu kwamba amepokea taarifa zinazoonesha kuwa ameshinda kwa kiwango kikubwa.Aliwaambia waandishi wa habari kuwa taarifa hizo zimepokewa kutoka taasisi zote za Gabon na nje ya nchi.

Jumapili kiongozi wa upinzani wa muda mrefu Pierre Mambouddou na waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani Andre Mba Obame pia walisisitiza kuwa walipata ushindi wa takribani kura zote. Matokeo ya awali yanatarajiwa kutolewa baadaye leo. Baadhi ya wafuasi wa upinzani wanasema wanahofu ghasia huwenda zikatokea na shutuma za kuwepowizi wa kura kama Bongo anatangazwa mshindi.

Gabon ina mfumo wa raundi moja tu ya uchaguzi. Mgombea anayepata kura nyingi anatangazwa mshindi, na hakuna duru ya pili ya uchaguzi inayohitajika.Uchaguzi ulifanyika baada ya kifo cha mwezi June cha rais Bongo, aliyekuwa na umri wa miaka 73 na ambaye aliiongoza nchi kwa zaidi ya miaka 41.