Wabunge Kenya wataka ateuliwe Mkuu wa shughuli za Serikali Bungeni

Wabunge nchini Kenya wameanza harakati za kutafuta kiongozi rasmi wa shughuli za Serikali bungeni, baada ya Serikali kushindwa kuelezea nani ni kiongozi wa shughuli hizo, kati ya Waziri Mkuu, Raila Odinga na Makamu Rais, Kalonzo Musyoka.

Wabunge wanasema hali hiyo imeathiri shughuli za bunge huku mawaziri wakishindwa kujibu maswali, licha ya shutuma kutoka kwa Spika. Viongozi hao wamezidisha shughuli za kumtafuta kiongozi rasmi atakayesimamia shughuli za Serikali katika bunge kupitia mswaada unaolenga kutatua mzozo huo.

Pia wabunge hao wanasema mivutano kati ya viongozi katika Serikali ya Muungano imerudisha nyuma utendaji kazi wa shughuli za bunge, kwani baadhi ya mawaziri wamekuwa wakikataa kujibu maswali na hata kukwepa kufika bungeni kama inavyotakiwa.

Mbunge wa Kigumo, Jamlek Kamau ambaye ndiye mdhamini wa mswaada huo amesema hatua ya Rais Mwai Kibaki na Waziri Mkuu, Raila Odinga kushindwa kutatua mzozo huo imechangia katika juhudi zilizofikiwa sasa na wabunge.

Bwana Kamau amesema licha ya msimamo huo wabunge bado wana imani kuwa Rais na Waziri Mkuu watalitatua suala hilo.