Vurugu zaendelea Somalia

New York - Umoja mataifa umesema watu laki mbili na ishirini na tatu elfu wameukimbia mji mkuu wa Somalia, Mogadishu tangu mapigano kuzuka tena kati ya wanamgambo wa ki-Islam na majeshi ya serikali mwezi Mei. Shirika la kuhudumia wakimbizi la umoja mataifa liliripoti leo Jumanne kuwa raia elfu ishirini wa Somalia wamekimbia katika muda wa wiki mbili zilizopita pekee. Msemaji Ron Redmond alielezea wasiwasi kuhusu idadi kubwa ya watu waliokoseshwa makazi wanaotafuta hifadhi kwenye maeneo ya Afgooye, kusini-magharibi ya mji mkuu. Eneo hilo tayari lina hudumia wakimbizi laki nne kutoka mapigano ya awali.