Kufuatia kuibuka kwa makundi ya kigaidi nchini Somalia na Kenya. Serikali ya Kenya imeanza kuchunguza madai kuwa vijana wanaanza kuandikishwa kujiunga na kundi la kigaidi la Somalia Al-Shabaab.
Lakini nchini Kenya, inaripotiwa mkenya kwa jina Saleh Ali Saleh Nabhan anaongoza kundi lake la kigaidi lenye ushirika na mtandao wa kigaidi wa al Qaida kwa jina Al-Muhajirun. Kundi lake hilo yaripotiwa lina wapiganaji waliopewa mafunzo nchini Afghanistan na Pakistan.
Akizungumza na sauti ya Amerika kutoka Mombasa, mwenyekiti wa baraza kuu la mashauri la waislam wa Kenya Sheikh Juma Ngao, alisema viongozi wa dini ya kiislam wanajiandaa kutoa hamasa kwa waislamu kote nchini humo kupitia misikiti na madrassa kuwaelezea vijana misingi na nguzo za dini ya kiislam ambayo inalaani vikali vitendo vyote vya kigaidi.
Aidha Sheikh Ngao alisema hivi karibuni baraza lake litaanda kukutana na familia ya Saleh Nabhan kusikiliza maoni yao na kutoa ushauri kwao kufutia tendo la kijana huyo kujihusisha na vitendo vya kigaidi. Nabhan anatuhumiwa kuhusika na jaribio la kutungua ndege ya Israel ikiwa katika anga ya Kenya na hoteli ya Paradise mjini Mombasa .
Na kuhusu ombi la Somalia kuzitaka nchi jirani za Kenya, Djibouti, Ethiopia na Yemen kupeleka majeshi yao kusaidia serikali dhaifu ya Somalia, Sheikh Ngao alisema haungi mkono ombi hilo. Alisema kupeleka majeshi hayo nchini Somalia ni kuhatarisha maisha yao bure na kwamba tatizo la kisiasa la Somalia linapaswa kutatuliwa na wasomalia wenyewe, kwani ni watu wa kabila moja, lugha moja na dini moja.