Mahakama ya Rwanda Yakataa Madai ya Nkunda

  • Daniel Gakuba

Jenerali Laurent Nkunda ambaye aliingia nchini Rwanda akikimbia oparesheni ya pamoja dhidi ya makundi ya waasi mashariki mwa Congo iliyofanywa na majeshi ya DR Congo, Rwanda na Uganda, alikamatwa na kutiwa nguvuni mara tu baada ya kuingia Rwanda.

Tangu wakati huo amekuwa akishikiliwa eneo la siri nchini humo, na wiki chache zilizopita alifungua kesi katika mahakama ya wilaya ya Nyarugenge akilishitaki jeshi la Rwanda kuwa lilimkamata na kumshikilia kinyume cha sheria. Lakini mahakama hiyo iliyakataa madai hayo na kusema mawakili wa Nkunda hawakuwa na ushahidi wa kutosha.

Nkunda alifungua kesi nyingine katika mahakama ya Gisenyi akilishitaki jeshi la Rwanda, lakini kwa mara nyingine tena kesi hiyo imetupiliwa mbali na mahakama hiyo kwa maelezo kuwa mawakili hao walishindwa kueleza ni wapi mteja wao anashikiliwa na anashikiliwa na nani.

Wakati serikali ya Rwanda inasema kuwa Nkuda alikamatwa akikimbia mapigano mashariki mwa Congo, mawakili wake wanadai kuwa Nkunda alikamatwa wakati alipohudhuria mkutano baada ya kupata mwaliko rasmi kutoka maofisa wa jeshi la Rwanda.