Nkunda Ashitaki Jeshi la Rwanda

Jenerali Nkunda kupitia mawakili wake amelifikisha mahakamani jeshi la RPF kwa madai kuwa lilimteka nyara na kumweka kizuwizini kinyume cha sheria wakati alipoingia nchini humo akitokea uwanja wa vita mashariki mwa Congo-Kinshasa.

Lakini waziri wa ulinzi wa Rwanda alitarajiwa kufika mahakamani akiliwakilisha jeshi, lakini hakuonekana na hakuna maelezo yaliyoweza kupatikana kuhusu sababu zilizopelekea kushindwa kwake kuwepo mahakamani.

Hatahivyo, wawakilishi wa serikali katika kesi hiyo, waliwaandama kwa mara nyingine mawakili wa Nkunda wakisema kuwa mahakama walipofungua kesi hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo.

Wakati huo huo, mbunge wa Masisi Kivu ya Kaskazini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Destali Kizinkiko, anasema Nkuda inabidi arudishwe nchini Congo kukabiliana na mashitaka ya uhalifu wa kivita.

Kizinkiko anasema kuwa Nkunda ni raia wa Congo na kwamba uhalifu aliufanya nchini Congo. Kutokana na sababu hizo alisema inabidi afikishwe katika mahakama ya Congo.