Baraza la Mawaziri Kenya Lameguka

Waziri wa Sheria na Maswala ya Katiba nchini Kenya Martha Karua amejiuzulu baada ya kuhitilafiana na Rais Mwai Kibaki na serikali kwa ujumla kuhusu marekebisho katika idara ya sheria na mahakama. Martha Karua amesema kuwa amelazimika kujiuzulu baada ya kupuuzwa na kuzuiliwa kutekeleza majukumu yake kama waziri wa sheria.

Mwandishi wa Sauti ya Amerika aliyepo Nairobi anasema uamuzi wa Bi. Karua kujiuzulu haukuwashangaza wengi kutokana na mvutano uliokuwepo kati yake na serikali ya Kenya. Anasema hivi karibuni serikali ya Rais Mwai Kibaki ilionyesha kupuuza maswala yanayohusu wizara yake.

Hivi karibuni Rais Mwai Kibaki aliwateua majaji wakuu bila kumshirikisha Martha Karua ambaye alikuwa waziri wa sheria. Baadhi ya wananchi wa Kenya wamepongeza uamuzi wa Bi. Karua kujiuzulu kwa maelezo kuwa inaonyesha maadili mazuri na hali ya kutokuwa na uchu wa madaraka.